RM, 01/03/2018
Jumuiya ya Maendeleo ya Wana-Busega waishio nje ya Busega, BUDECO (Busega Development Community) imepongezwa na mkuu wa wilaya ya Busega Bi. Tano Seif Mwera kwa kutoa mchango wa fedha taslimu Shilingi 34,700,000/= kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa katika wilaya ya Busega.
Mchango huu uliwasilishwa rasmi siku ya Jumatatu tarehe 26/02/2018 katika ofisi ya mkuu wa wilaya na Mwenyekiti wa Jumuiya ya BUDECO Bw. Maselle Joseph Ginhu kwa kushirikiana na mwakilishi wa wanachana waishio karibu na Busega, Dr. Simon Songe.
Mkuu wa wilaya ya Busega Bi. Tano Mwera akimkabidhi hati ya shukurani Mwenyetiki wa BUDECO Bw. Maselle Joseph Ginhu. Aliyesimama katikati ni Dr Simon Songe.
Katika hafla hiyo fupi ya makabidhiano ya mchango huu ambayo ilishuhudiwa pia na viongozi mbalimbali wa wilaya ya Busega, mkuu wa wilaya Bi. Tano Mwera alinukuliwa akisema:
“Kwa niaba ya wilaya ya Busega nawashukuru sana wana-BUDECO kwa mchango huu wa kuchangia ujenzi wa vyumba vya madarasa katika wilaya yetu ya Busega.”
Aliendelea kwa kuwahimiza wadau wengine kuona umuhimu wa kuchangia sekta ya elimu ili kutatua changamoto ya miundombinu iliyopo katika shule za msingi na za sekondari. Akiahidi kusimamia vizuri matumizi ya mchango huu alisema: “Natumia nafasi hii pia kuahidi michango hii tutaifuatilia na kuisimamia kwa karibu sana ili kuhakikisha kwamba inatumika vizuri kwa ujenzi kama ilivyokusudiwa ili kuweza kuwanufaisha wanaBusega na Watanzania kwa ujumla.”
Akikabidhi msaada huu, mwenyekiti wa BUDECO -- Jumuiya ya Maendeleo ya Wana-Busega -- Bw. Maselle Joseph Ginhu alisema; Kwa kutokana na changamoto zinazoikabili sekta ya elimu katika Wilaya ya Busega, wanachama wa BUDECO waliamua kukaa kikao na kuchangishana na kisha kupata kiasi hicho cha fedha ili kuwaokoa wanafunzi waliobaki nyumbani kwa kukosa vyumba vya madarasa. Bwana Ginhu alinukuliwa akisema: “Sisi wanaBusega tuishio nje ya Busega tuliguswa na hilo, hivyo tukaamua kuchangishana. Tumeweza kukusanya shilingi milioni 34.7 ambazo leo tumezikabidhi kwenye ofisi ya wilaya na mbele ya viongozi wa halmashauri ya Wilaya ya Busega ili ziweze kwenda kutekeleza ujenzi wa hayo madarasa ambayo yalikuwa yamekwamisha wanafunzi.”
Mwenyekiti wa jumuiya ya WanaBusega Bw. Masele akifafanua shughuli za BUDECO kwa viongozi wa wilaya ya Busega
Itakumbukwa kuwa wilaya ya Busega ni miongoni mwa wilaya zilizofanya vizuri katika matokeo ya mtihani wa darasa la saba mwaka jana (2017) katika mkoa wa Simiyu, lakini bado kuna idadi kubwa ya wanafundi ambao hawajajiunga na kidato cha kwanza kwa kutokana na changamoto za miundombinu hususani upungufu wa vyumba vya madarasa.
Mchango huu kwa ajili ya ujenzi wa madarasa wilayani Busega ni baadhi tu ya shughuli za kimaendeleo zinazofanywa na jumuiya ya BUDECO (Busega Development Community). Aidha BUDECO ni shirika lisilo la kiserikali, kidini wala kikabila. Malengo yake yameainishwa vizuri katika Katiba ya shirika hili, hususani katika maelezo ya dira, dhima na madhumuni yake kwamba ilisajiliwa rasmi tarehe 15/Oktoba/2013 kwa lengo la kuchangia shughuli za Maendeleo, kuhamasisha na kuijengea uwezo jamii ya WanaBusega ili kutumia rasilimali zilizopo kwa lengo la kuinua hali ya maisha ya kijamii, kiuchumi na kiutamaduni.
Kwa maelezo zaidi tafadhali tembelea tovuti rasmi ya jumuiya hii www.budeco.co.tz
# Video ya makabidhiano ya mchango wa ujenzi wa miundombinu ya shule katika wilaya ya Busega:
WebM media format: Makabidhiano ya mchango wa ujenzi wa madarasa wilaya ya Busega
# Picha nyinginezo za makabidhiano ya mchango wa ujenzi wa madarasa katika wilaya ya Busega:
___
Maelezo ya ziada kwenye makala haya na video yametoka kwa:
Bw. Shaban Lupimo (StarTV) na Bw. Joel Shushu (Magazeti ya serikali)